Jumatatu 15 Juni 2026 - 22:08
Uingereza Inashirikiana na Watawala wa Bahrain katika Kuwakandamiza Mashia wa Nchi Hiyo

Hawza/ Shirika la “SALAM” limesisitiza kwamba; sera za Uingereza zimechangia kuimarisha mifumo ya ukandamizaji na kutoadhibiwa kwa wahusika nchini Bahrain, badala ya kuleta mageuzi ya kweli katika suala la haki za binadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Shirika la SALAM la Demokrasia na Haki za Binadamu nchini Bahrain limesisitiza kwamba; sera za Uingereza zimechangia kuimarisha mifumo ya ukandamizaji na kutoadhibiwa kwa wahusika nchini Bahrain, badala ya kuleta mageuzi halisi katika faili la haki za binadamu.

Shirika hilo katika ripoti iliyochapishwa kwenye tovuti yake chini ya anuani ya “Nyuma ya Milango Iliyofungwa; Uchambuzi wa Athari za Uingereza kwa Haki za Binadamu nchini Bahrain”, limesema kuwa; serikali mbalimbali za Uingereza zimekuwa zikiweka mbele maslahi ya kimkakati, kiuchumi na kiusalama kuliko masuala ya haki za binadamu, licha ya ahadi zao za mara kwa mara na za wazi za kuimarisha mageuzi nchini Bahrain.

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa msingi wa uchambuzi mpana wa diplomasia ya Uingereza, ushirikiano wa kiusalama, sera za biashara, programu za msaada wa taasisi pamoja na mifano ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu binafsi.

Shirika hilo liliongeza kwamba; tangu kuzuzuiwa maandamano ya kutaka demokrasia nchini Bahrain mwaka 2011, nchi hiyo imeshuhudia mchakato endelevu wa kudhoofika kwa haki za kiraia na kisiasa, hali hiyo imejumuisha kuvunjwa kwa makundi ya upinzani, kufungwa kwa vyombo huru vya habari, na kuendelea kuzuiliwa viongozi wa kisiasa, wanazuoni wa dini na watetezi wa haki za binadamu. Aidha, mashirika ya kimataifa yameandika na kuthibitisha matukio ya mateso, kesi zisizo za haki na kutoadhibiwa kwa wahusika, kwa mujibu wa shirika hilo, hali hii ya kuzorota imeendelea sambamba na uungaji mkono wa pande mbalimbali wa Uingereza kwa washirika wake wa Bahrain.

Shirika hilo pia lilibainisha kwamba; vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza vimeongezeka zaidi mwaka 2026, kwa mujibu wa ripoti zilizopo, mamlaka ya Bahrain imewakamata takriban watu 300 kwa sababu ya kutoa maoni katika mitandao ya kijamii, kushiriki katika maandamano na shughuli za kisiasa zinazohusiana na maendeleo ya eneo hilo pamoja na mgogoro uliowahusisha Iran, utawala wa Kizayuni na Marekani.

Ripoti hiyo iliongeza kwamba; ushirikiano wa Uingereza haujaweza kuboresha hali ya haki za binadamu nchini Bahrain, wakati huo huo, masuala ya haki za binadamu yamekuwa hayapo katika mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili, huku ushirikiano wa kiusalama na msaada wa taasisi kutoka Uingereza kwa taasisi za Bahrain ukiendelea, licha ya taasisi hizo kutuhumiwa kwa kufanya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha